Maajabu! Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Spirit and Truth, Amani Rubeni Mirumbe ameushangaza ulimwengu kwa kujitabiria kifo na baadaye kufariki dunia kweli huku akiwaachia waumini na familia yake wosia wenye viashiria vya kuzikwa Kiislam, Amani linakujuza.
Kifo hicho kilijiri saa 3:12 asubuhi ya Machi 24, mwaka huu, Mabibo jijini Dar es Salaam mahali lilipo kanisa na nyumba ya mchungaji huyo na kuzikwa saa 10:21 jioni. Kwa maana hiyo, mwili huo ulikaa kwa saa saba tu.
KILICHOSABABISHA KIFO
Saa chache baada ya kifo, Amani lilifika msibani na kufanikiwa kubaini mawili matatu kuhusu kifo cha mtumishi huyo wa Mungu.
Kwa mujibu wa mmoja wa waumini wake, marehemu Mchungaji Mirumbe alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya presha lakini asubuhi ya siku ya tukio, alipoamka alimwita msaidizi wake na kumwambia siku hiyo haiwezi kupita bila yeye kukata roho.
“Ni ajabu sana, alipoamka tu alimwita msaidizi wake, akamwambia siku ya leo (Jumatatu) lazima afe ila kabla ya kuiacha dunia anataka kuacha wosia wake kwa ajili ya familia na sisi waumini,” alisema muumini mmoja ambaye aliomba hifadhi ya jina.
WOSIA NI HUU
Muumini huyo alisema kuwa, mchungaji huyo akiwa katika hatua za mwishomwisho kabla ya kifo, aliacha wosia kwamba, akishakata roho hatataka mwili wake uzikwe ukiwa ndani ya jeneza kama wafanyanyiwavyo Wakristo au wachungaji wengine.
“Marehemu aliagiza mwili wake uwekwe kwenye sanda na hata kama ataagwa zoezi hilo lifanyike mwili ukiwa ndani ya sanda ambayo itazungushiwa mkeka,” muumini huyo alizidi kuanika wosia huo.
KUHUSU MAITI YAKE
Katika wosia huo, Mchungaji Mirumbe aliagiza maiti yake isilale hata usiku mmoja na wala isisafirishwe kwenda kwao mkoani Mara kwa mazishi.“Alisema akitokea mtu kimbelembele na kujiamulia kuisafirisha maiti yake kwenda kuzikwa kokote nje ya Dar, basi ajue atarudi nayo atake asitake,” kilisema chanzo.
HAKUNA KULIA
Mwisho marehemu huyo hakutaka waumini wake wale familia yake kumwaga machozi kufuatia kifo chake kama njia ya kuomboleza.
WAUMINiWAUPOKEA MWILI
Amani liliwashuhudia waumini wa kanisa hilo wakiupokea mwili wa mchungaji wao kutoka ndani ya nyumba yake ulikokuwa umehifadhiwa baada ya kifo ukiwa umeviringishwa kwenye mkeka na kupelekwa kanisani kwa ajili ya kuombewa na kuagwa kabla ya kupelekwa makaburini.
Wakati wa kuuaga mwili, baadhi ya ndugu na waumini wachache walionekana kuvunja wosia wa mchungaji huyo ambapo walionesha wazi masikitiko yao kwa kuangua vilio licha ya kuonywa na baadhi ya viongozi.
HALI YA MAKABURINI
Mwili huo ukiwa ndani ya sanda iliyozungukwa na mkeka uliwekwa juu ya meza ndani ya kanisa lake. Baada ya zoezi hilo, ndugu na waumini waliuchukua mwili huo hadi kwenye Makaburi ya Ubungo Fishnet Industry ‘Ufi’, Shekilango jijini Dar kwa mazishi ambapo mwili uliingizwa kwenye mwanandani.
Baadhi ya ndugu na waumini walisimamia wosia kuhakikisha hakuna kisichofuatwa ambapo walisimamia zoezi la kumzika mchungaji huyo pasipo kitu chochote zaidi ya sanda tu kama alivyoagiza.
MTOTO WA MAREHEMU ANENA
Akizungumza na mwandishi wetu makaburini hapo, mtoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Adam Mirumbe alithibitisha utabiri wa kifo na wosia wa baba yake kwa msikitiko.
“Kweli baba aliniambia kuwa angekufa leo na
alinipa wosia kuwa maiti yake isilale, isisafirishwe, watu wasilie
msibani na kubwa zaidi ni kwamba azikwe bila jeneza, yaani na sanda tu
kama ulivyoona. Unaweza kusema amezikwa Kiislam, lakini yeye aliamini
atakuwa amezikwa kama Yesu,” alisema mtoto huyo.
KUHUSU MKE WA MAREHEMU
Adam aliongeza kuwa, wakati kifo cha baba yake kinatokea, mama yake hakuweza kuhudhuria kwa sababu alikuwa safarini kuelekea Musoma, Mara kwenye msiba wa mtoto mwingine ambapo maziko yake ilibidi yasimamishwe mpaka mwili wa mchungaji huyo uhifadhiwe kwenye nyumba yake ya milele.
KUMBE NI BABA WA MSANII WA BONGO MUVIKUHUSU MKE WA MAREHEMU
Adam aliongeza kuwa, wakati kifo cha baba yake kinatokea, mama yake hakuweza kuhudhuria kwa sababu alikuwa safarini kuelekea Musoma, Mara kwenye msiba wa mtoto mwingine ambapo maziko yake ilibidi yasimamishwe mpaka mwili wa mchungaji huyo uhifadhiwe kwenye nyumba yake ya milele.
Mwandishi wetu aliwashuhudia wasanii wa filamu Bongo ‘Bongo Movies’, Mohammed Mwikongi ‘Frank’ na Michael Philip ‘Kojaki’ wakimtia nguvu msanii mwenzao ambaye ni mtoto mmojawapo wa mchungaji huyo ambaye kisanii anajulikana kwa jina la Mgomakufa.
KWA NINI KIISLAM?
Baadhi ya watu waliohudhuria msiba huo walishindilia utaratibu huo kuwa ni wa imani ya Kiislam wakidai kwamba, mwili huwa haulali (labda dharura), hauzikwi ukiwa ndani ya jeneza (sanduku) na huwekwa kwenye mwanandani.
“Sijui kwa nini mchungaji aliamua kutoa wosia huo? Huenda kuna kitu alikiona ambacho kilimpa ishara kwamba, kuzikwa ndani ya jeneza na maiti yake kulala kuna mambo atayakosa mbele ya safari akhera,” alisema mwombolezaji mmoja.
MAZISHI YA KIKRISTO
Katika utaratibu wa mazishi ya Kikristo, mwili huhifadhiwa ndani ya jeneza, unaweza kulala hata siku tatu bila kuzikwa, hakuna mwanandani kwa sababu mwili unakuwa ndani ya sanduku.
Post a Comment