SAFU ya marafiki, inayojadili mambo ya kirafiki na wadau wa rika zote ambao kwa kiasi kikubwa wamebadilishwa fikra zao kwa kuwa wafuasi wa hapa.
Yes! All About Love iko hewani. Kama ndiyo mara ya kwanza unapitia ukurasa huu, umefika sehemu sahihi sana ya kukupa elimu kwa undani kuhusu uhusiano, maisha na mapenzi. Karibuni.
Vilio vya wasichana wengi wenye umri wa kati (hasa kuanzia 24 – 30) ni kuhusu kuachwa baada ya kukaa na wapenzi kwa muda mrefu wakiwa na ahadi ya kuolewa. Wenyewe wanasema wanapotezewa muda.
Hapa kuna makundi mawili, la kwanza ni kwa wale ambao wamedumu kwa muda mrefu (kuanzia miaka miwili na kuendelea) kisha wanaachwa na kundi la pili ni wale ambao wanaachwa baada ya muda mfupi na kwenda kwa mwingine.
TATIZO LIKO WAPI?
Ni kweli kwamba inauma sana kuwa na mtu kwa muda mrefu ukiwa na matarajio ya ndoa halafu baadaye unaachwa ghafla. Jambo hilo linauma sana lakini ni vizuri sasa kuangalia kwenye tatizo.
Wasichana wengi hukosea mitindo ya maisha, tabia na mengineyo ambayo kwa kiasi kikubwa huchangia kuachwa baada ya muda mfupi tangu kuanzisha uhusiano au ghafla baada ya kipindi kirefu cha uhusiano.
WANAPOKOSEA (WANAOACHWA NDANI YA KIPINDI KIFUPI)
Kwa bahati mbaya wasichana wengi wa sasa hujisahau na kuishi katika staili ambayo si halisi bali maigizo. Ndugu zangu, kuna tofauti kubwa sana kati ya mwanamke na mke.
Msichana ambaye ana matarajio ya kuwa mke, anatakiwa kuishi kama mke wa mtu mtarajiwa kweli. Ishi katika njia sahihi inayompasa mwanamke anayejitambua.
Tangu awali, wanawake wa kundi hili hukosea. Mfano, utakuta mwanamke anavaa mavazi ya kubana sana na kuchoresha mwili wake – kinachotokea hapo, mwanaume akimuona ni kumtamani tu na siyo kumpenda!
Sawa, inawezekana ukawa umevaa hovyo, lakini ukapendwa kiasili, ila sasa mwanaume husika ataogopa maana atakuhukumu kwa mavazi yako. Anaweza kuishia kusema: “Msichana mzuri sana, nimempenda lakini kwa alivyo, hafai kuwa mke, anaonekana hajatulia.”
Hata kama akizidiwa sana na hisia, anaweza kuamua kuingia kwenye uhusiano na wewe kwa lengo la kuifurahisha tu nafsi yake. Ndani ya muda mfupi sana, unaachwa.
Hapo sasa unakwenda kwa mwingine ambaye naye baada ya muda mfupi anakuacha kwa sababu zilezile. Hebu jiulize, utaachwa na wangapi.
Fanya utafiti wako taratibu, utagundua kuwa, wanawake wanaojiheshimu, hata kama mitaani huonekana washamba, ndiyo ambao barua za posa hutembea zaidi majumbani mwao.
TAMAA YA FEDHA
Mwanamke msumbufu wa fedha ana nafasi ndogo ya kupata mume. Mwanaume anapenda zaidi kutoa zawadi kwa mwenzi wake kwa matakwa yake au kama akitakiwa kutoa kitu fulani basi kiwe na ulazima.
Wapo baadhi ya wanawake, kazi yao mizinga. Kila kitu anataka kununuliwa na mwanaume. Mara saluni, mavazi, manukano nk. Kabla ya kuwa naye ulikuwa ukiishi vipi?
Mambo hayo kwa kweli huwakimbiza wanaume. Wao hupenda mwanamke ambaye humjali, humsaidia mawazo ikiwezekana hata namna ya kuanzisha biashara mpya kwa maendeleo ya baadaye.
HESHIMA YA NDANI
Angalia pia kauli zako, acha dharau. Kuwa msikivu na umpe mwenzi wako nafasi ya kwanza kwenye mambo yako. Acha kumkosoa kwa kumkaripia. Kama kuna jambo unadhani analikosea, kuwa mzungumzaji mwenye unyenyekevu.
Mwanaume anapenda kuheshimiwa, maana yake kama ukiwa mkali au husikii, hawezi kukupa nafasi ya kuwa mke.
Wiki ijayo tutaangalia kundi la pili, wale wanaochwa baada ya uchumba wa muda mrefu, USIKOSE!
Post a Comment