Siyo tetesi tena. Sasa ni rasmi kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amekuwa akitajwa kuwania urais amethibitisha wazi kuwa atagombea kiti hicho katika uchaguzi mkuu mwakani.
Alitoa uthibitisho huo juzi akiwa London,
Uingereza ambako yuko katika shughuli za kikazi. Hatua hiyo inaondoa
uvumi ambao umekuwapo kwa takriban miezi mitatu sasa kwamba naye tayari
ameingia katika kinyang’anyiro hicho.
Pinda aliweka wazi nia ya kuelekea Ikulu
akisisitiza kuwa hajatangaza rasmi lakini akasema kuwa ameanza harakati
hizo ‘kimyakimya’. Alikuwa akijibu moja ya maswali aliyoulizwa katika
Kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la
Uingereza (BBC).
Alitamka rasmi kuwania nafasi hiyo baada ya
kuulizwa kuwa anafikiri ni kiongozi gani anayefaa kurithi mikoba
itakayoachwa na Rais Jakaya Kikwete.
“Mikoba ya Rais Kikwete inaweza kuchukuliwa na
yeyote atakayeonekana mwisho wa safari kwa utaratibu wa chama na ndani
ya Serikali .... kama anafaa. Waliojitokeza sasa ni wengi na mimi
ninadhani ni vizuri,” alisema Pinda.
Alipoulizwa kama yupo miongoni mwa wengi alisema,
“… umesikia kama nimo … basi tukubali hilo na yeye Waziri Mkuu yumo. Hao
wote waliojitokeza pamoja na Waziri Mkuu aliyejitokeza ni katika
jitihada za kusema hebu Watanzania nitazameni je, mnaona nafaa au
hapana?”
“……..fanyeni hivyo kwa mwingine na mwingine,
mwisho wa yote zile kura zitakazopatikana kwenye mkutano mkuu kama ni
kutokana na chama kile kinachotawala na hatimaye Watanzania
watakaojitokeza kupiga kura Oktoba kutokana na wagombea watakaojitokeza
kutoka kwenye vyama mbalimbali huyo ndiye tutakayempata kama rais. Hivyo
natangaza nia hiyo kimyakimya.”
Kiongozi huyo atakuwa wa pili kutangaza nia hiyo
kupitia vyombo vya habari vya kimataifa, baada ya Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Alitangaza nia hiyo Julai 2, 2014, alipokuwa
Uingereza katika mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa
kwenye kipindi hicho hicho cha Dira ya Dunia.
Urais CCM
Kuingia kwa Pinda katika mbio za urais kupitia CCM
tayari kumebadili mwelekeo wa kinyang’anyiro cha nafasi hiyo kubwa ya
uongozi nchini kutokana kuzigawa baadhi ya kambi za wagombea ambao
walikuwa wakitajwa kwa muda mrefu kabla yake.
Wengine ambao wamekuwa wakitajwa kuwania nafasi
hiyo kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu
Mstaafu Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu),
Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),
Steven Wassira, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla.
Nguvu ya Pinda
Baadhi ya wapiga debe wa Pinda wakiongozwa na
Mwenyekiti wa Mamlaka za Mitaa Tanzania (Alat), ambaye pia ni Meya wa
Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, wamekuwa wakiweka kambi zao
Dodoma kila kunapokuwa na vikao rasmi vya CCM ili kuwashawishi wajumbe
wa vikao vya juu vya chama hicho wamuunge mkono.
Wakati wa vikao vya CC na NEC vya CCM
vilivyomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma, kundi la wafuasi wa Pinda
likiongozwa na Dk Masaburi lilikuwa mjini humo kuendelea na jitihada za
kusaka wafuasi.
Harakati hizo zinaweza kuwa ndiyo maana ya kauli
ya Pinda pale aliposema kwamba tayari ametangaza ‘kimyakimya’ nia yake
ya kugombea nafasi hiyo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Dk Benson Bana anaunga mkono msimamo wa Pinda na wengine waliojitangaza
katika chama chake huku akivilaumu vyama vya upinzani kwa wagombea wao
kukaa kimya badala ya kujitokeza ili wananchi wawapime kama wa CCM
wanavyofanya.
Kuhusu Pinda, Dk Bana alisema: “Ni mzoefu amekaa
Ikulu muda mrefu na kwa wadhifa wake, si vibaya kujitangaza kwani
anayejitangaza wananchi wanapata muda wa kumpima na chama pia kinampima
tofauti na wale ambao hawajitangazi ambao ni hatari sana kwa kuwa
wanapita chinichini kutoa rushwa.”
Kuhusu upinzani, alisema: “Sijui upinzani wana
matatizo gani, ningefurahi kuona (Halima) Mdee, (John) Mnyika au
(Willbrod) Dk Slaa wanajitokeza ili wananchi wawapime kwani Dk Slaa wa
2010 siyo Dk Slaa wa sasa. Wakijitokeza italeta uhai kwenye hizi
harakati na wananchi watakuwa na nafasi nzuri ya kuwapima,” alisema na
kuongeza: “Upinzani wanapokaa kimya wanatunyima fursa wananchi
kuwapima.”
Manung’uniko
Tangu kuanza kwa tetesi kwamba Pinda ameingia
katika kinyang’anyiro cha urais, kumekuwa na malalamiko ya chinichini
dhidi yake kwamba amekuwa akicheza rafu kama ambazo ziliwafanya na
makada wenzake wenye nia sawa na yake kufungiwa na Kamati Kuu ya CCM.
Itakumbukwa kwamba makada sita wa chama hicho
ambao ni Sumaye, Lowassa, Membe, Makamba, Wasira na Ngeleja wanatumikia
adhabu na wapo chini ya uangalizi wa chama hicho baada ya kutiwa hatiani
kwa makosa ya kuanza kampeni za urais kabla ya muda kutangazwa.
Baadhi ya wagombea na makada wa CCM wamekuwa
wakidai kuwa Pinda naye anacheza rafu hivyo kutaka ashughulikiwe, lakini
wengine wamekwenda mbali zaidi na kuhoji ushiriki wake katika Kikao cha
Kamati Kuu ambacho kilitoa adhabu hiyo ilhali akijua kwamba naye
atakuja kugombea.
Makamba, Kigwangalla
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kikwangalla
wamesema wanamkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika mpambano wa
kuwania safari ya kwenda Ikulu kupitia CCM.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, Makamba na
Kigwangalla walionekana kutostushwa na uamuzi wa Pinda kuingia rasmi
katika mbio hizo huku wakisema siyo tishio kwao.
Makamba kwa upande wake alisema hakuna cha ajabu
kwa Pinda kuwania nafasi hiyo kwani 1995 alijitokeza Cleopa Msuya ambaye
alikuwa pia waziri mkuu kupambana na mawaziri wengine kama Jakaya
Kikwete na Edward Lowassa lakini alishindwa na Benjamin Mkapa ambaye
alipitishwa.
Alisema pia mwaka 2005 alijitokeza Waziri Mkuu, Frederick Sumaye dhidi ya mawaziri wengine wadogo, lakini walimshinda.
“Mara zote hizo wagombea wengine walifanikiwa
dhidi ya mawaziri wakuu. Nafasi za madaraka ya kiserikali hazina nafasi
katika uteuzi wa wagombea ndani ya CCM,” alisema Makamba.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli alisema
anamkaribisha ili wapimane ubavu lakini akasema ni muhimu kuanzia sasa
hadi Mei mwakani, harakati hizo zisiathiri kazi za Serikali hasa
ikizingatiwa kuwa Pinda ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali.
Dk Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayosimamia
Ofisi ya Waziri Mkuu alisema haogopi mgombea hata mmoja, hata akiwa na
cheo kikubwa au kidogo kwake si tishio.
“Waziri Mkuu anakaribishwa kwenye mbio hizi na
asifikiri zitakuwa rahisi kwani watu tumejipanga na tuna mikakati ya
kushinda,” alisema Kigwangalla.
Hata hivyo, Dk Kikwangalla alisema kuingia kwa
Pinda kunaweza kuharibu mchakato mzima kwenye chama kwa kuwa ni mmoja wa
watu wanaotoa uamuzi hasa ikizingatiwa kuwa kwa nafasi yake, anaingia
kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.
“Waziri Mkuu yuko kwenye nafasi ya kutuchuja,
hivyo ni kama kusema refa ameamua kucheza kitu ambacho ni tatizo.
Kitendo cha kutaka uongozi katika nafasi kama yake kitaondoa usawa,”
alisema Dk Kikwangalla.
Post a Comment