Katika hali ya kawaida, binti wa miaka 11 (jina linahifadhiwa
kwa sababu za kimaadili), mkazi wa kijiji cha Kongogo, Wilayani Bahi
mkoani Dodoma hivi karibuni aliolewa na binamu yake, kisha ndoa yake
kuvunjwa na Serikali.
Hakuna taarifa nyingi za mabinti kuolewa katika
umri mdogo katika wilaya hiyo mbali ya kuwepo kwa watoto wadogo ambao
huondolewa katika masomo na wengine kushindwa kupata elimu kwa sababu
wazazi wao huwapeleka migodini na wengine maeneo ya mijini kutumikishwa
majumbani.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa,
anasema wilaya yake inaongoza mkoani hapa kwa kuwa na kiwango kikubwa
cha vitendo vya ukeketaji wa wanawake ikiwa nayo ni sehemu ya ukatili
wa kijinsia.
Lakini kwa tukio hilo, lililojitokeza katika moja
ya familia ya wafugaji, kunaweza kukafanya umuhimu wa kujikita katika
utafiti wa kina kuliangalia suala la kuolewa katika umri mdogo lina
ukubwa gani mkoani hapa.
“Hazungumzi na mtu yeyote humu ndani na unaweza
kumsemesha anakuangalia tu, ila anazungumza na mimi (Mkwasa), ama
wasichana wawili tu wa hapa ndani ambao anashinda nao,”anasema Mkwasa
ambaye sasa anamlea mtoto huyo.
Maneno hayo yanathibitishwa na mwandishi wa makala
haya, aliyefika nyumbani kwa Mkwasa kwa nia ya kuzungumza naye baada
ya kupata taarifa ya kuwepo kwa mtoto huyo.
Anapoitwa kwa nia ya kutambulishwa, anafika
mlangoni na kubaki akiangalia tu huku wakati mwingine akiinamisha macho
yake chini na hata anaposalimiwa haitikii, badala yake anaondoka na
kwenda kujificha ndani.
Hali hii iliweka ugumu katika kufanya mahojiano
naye, lakini kwa usiri mkubwa inatubidi kumtumia mmoja wa wasichana
ambaye amekuwa muwazi kwake kusikia nini kilichotokea.
Si kwamba hazungumzi, la hasha binti huyu ni
mzungumzaji mzuri na tunapotoka nje na kuwaacha wawili ndani ya sebule
hiyo tunawasikia wakizungumza na hata kucheka kwa sauti.
Mkwasa anasema siku za mwanzoni binti huyo
alikuwa haongei na mtu yoyote lakini baada ya kuhudumiwa na
mwanasaikolojia ambaye hufika nyumbani kwake kila baada ya siku tatu,
alianza kuongea.
Akisimulia tukio hilo, Mkwasa anasema mtoto huyo
alikutwa akizubaa na akiwa amechoka katika kijiji cha Mindola baada ya
kutoroka kwa mwanamume aliyeolewa naye
Anasema alipigiwa simu na viongozi wa kijiji hicho na kuagiza apelekwe katika kituo cha polisi.
“Nilikuwa kwenye kikao mjini, nikawaambia OCD
(Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Wilaya), akae naye mtoto huyo hadi
nitakaporejea, nilimwona mtoto. Hakuwa katika hali nzuri sana kwanza
alikuwa mwoga, halafu hakuwa anaongea na mtu yeyote,”anasema.
Anasema polisi walimshauri kumpeleka mtoto huyo
kwa daktari kwa ajili ya vipimo ambapo iligundulika kuwa ameshaingiliwa
sana kimapenzi na kuambukizwa magonjwa ya zinaa.
“Alipewa dawa na tukarudi nyumbani. Licha ya
kulalamika kuwa anasikia maumivu, hata kaa yake pale nyumbani kwa siku
za awali haikuwa nzuri,”anasema Mkwasa.
Anasema baada ya siku mbili mtoto huyo alionekana
anajisaidia haja ndogo iliyochanganyika na damu, hali iliyomfanya
kumrudisha tena hospitali alifanyiwa vipimo na kupewa dawa.