BAADA ya kuwepo malalamiko ya wasichana wadogo wa nchini kusafirishwa kwenda China kutumikishwa katika biashara ya ngono pamoja na dawa za kulevya, sasa serikali imenasa mtandao huo.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alitoa taarifa hiyo juzi
bungeni wakati akihitimisha michango kuhusu bajeti yake kwa mwaka wa
fedha 2014/15 iliyopitishwa.
Chikawe
ambaye hata hivyo hakufafanua kwa undani wa mtandao huo ulivyokamatwa,
alieleza Bunge namna watoto hao wanavyopatikana kabla ya kufikishwa nchi
hiyo ya nje.
Kwa
mujibu wa Waziri, watu hao wamekuwa wakichukua watoto wadogo na
kuwaambia kwamba wanawapeleka China hususani mji wa Guanzhou kuwaajiri
kwenye saluni na maduka.
Alisema
kinara wa usafirishaji amekuwa akitambuliwa kwa jina la ‘Mama’ ambaye
baada ya kufika nchini humo, huwanyang’anya watoto hao hati zao za
kusafiria. Imebainika zipo hata wakala zinazojihusisha na biashara hiyo
haramu ya binadamu.
“Wakifika,
Mama anawanyang’anya pasipoti zao. Anawaambia ili kuwarudishia, lazima
watimize masharti ya kumpa kati ya dola 8,000 na 10,000 baada ya
kutumika katika vitendo vya ngono,” alisema Waziri Chikawe.
Aliendelea
kueleza kuwa wanaposhindwa kutimiza masharti hayo, hukutana na
Wanigeria ambao huwapa hati bandia za kusafiria na kisha kuwaingiza
katika biashara ya kusafirisha dawa za kulevya kwenda nchi mbalimbali.
“Tumenasa
mtandao huu…polisi imenasa mtandao,” alisema Waziri na kutoa mfano
kwamba hivi karibuni, alikamatwa mtu akiwa na hati ya kusafiria
akimpelekea binti mmoja. Alisema binti huyo alipoulizwa juu ya hati
hiyo, alikuwa hafahamu anakokwenda.
Awali,
taarifa juu ya kuwepo usafirishaji wa wasichana wadogo kwenda China kwa
ajili ya kutumikishwa katika ngono, ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe baada ya kutoka ziarani
nchini humo.
Membe
alisema serikali inashirikiana na ubalozi wa China katika kubaini
wahusika wa biashara hiyo sanjari na mkakati wa kuhakikisha wasichana
hao wanarudishwa nchini.
Akielezea
mikakati ya serikali katika kukabili biashara haramu ya usafirishaji wa
binadamu, Waziri Chikawe alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014
Sekretarieti ya kupambana na biashara hiyo imeratibu vikao vinne vya
Kamati ya kupambana nayo.
Aidha
imeandaa kitabu cha anuani na majina ya watoa huduma kwa waathirika wa
biashara haramu ya usafirishaji binadamu na vilevile kutengeneza rasimu
ya kanuni za sheria ya kupambana na biashara hiyo nchini.
Katika
mwaka wa fedha 2014/2015 sekretarieti itakamilisha kutengeneza kanuni
za Sheria ya kupambana na biashara hiyo ya mwaka 2008. Pia itatoa elimu
na kuimarisha mikakati ya kupambana na biashara hiyo ya kusafirisha
binadamu.
Watanzania
zaidi ya 100 wakiwemo wasichana 20 wamedaiwa wapo gerezani nchini China
wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Post a Comment