MWAKA
2005 nilikuwa nikipanda daladala na Naseeb Abdul (Diamond) katika kituo
cha Shule Tandale Magharibi jijini Dar es Salaam. Wakati huo, sikuwa
hata na wazo kwamba atakuja kuwa mtu maarufu katika muziki hata
kushughulisha watu kutaka kujua zaidi kuhusu maisha yake.
Baada ya hapo nikaanza kuona wimbo wake wa kwanza kwenye video, ‘Nenda Kamwambie’ kilikuwa kibao kizuri kilichompa umaarufu, ndipo alipoanza kunivutia kusikiliza nyimbo zake. Baada ya video ile sikumuona tena kituoni kama ada yetu, nikaanza kusikia anaendesha gari aina ya Toyota Celica.
Kutoka mwaka 2006 mpaka sasa ni mfululizo wa mafanikio aliyoendelea kuyapata kijana huyu aliyezaliwa Septemba 28, 1988 mpaka kuwa mwanamuziki wa kwanza Tanzania kulipwa pesa nyingi kutokana na shughuli hiyo.
Kutokana
na utafiti uliofanywa na tovuti inayozungumzia masuala ya vijana
inasemekena ‘Diamond Platnamz’ anapata kiasi cha Sh Mil 16 kwa matamasha
mawili anayofanya katika mwezi.
Mbali ya mikataba minono aliyoingia na makampuni mbalimbali yanayonufaika kwa taswira ama sauti ya mwanamuziki huyo kijana, Diamond anaingiza fedha nyingi kila anaposafiri nje ya Tanzania na bara la Afrika kufanya matamasha ya muziki.
Mbali ya mikataba minono aliyoingia na makampuni mbalimbali yanayonufaika kwa taswira ama sauti ya mwanamuziki huyo kijana, Diamond anaingiza fedha nyingi kila anaposafiri nje ya Tanzania na bara la Afrika kufanya matamasha ya muziki.
Wakati
Diamond, ambaye hajatimiza hata miaka kumi kwenye tasnia ya muziki kuna
mtu mmoja anaitwa Muhidini Gurumo, amejishughulisha na muziki kwa
takriban miaka 45 lakini kila alipokutana na swali hili kutoka kwa
wanahabari kuwa kwa kipindi chote hicho muziki umemsaidia nini, jibu
lake ni: “Bado hakuna ninachoweza kujivunia kupitia muziki, hali ya
maisha ni ngumu.”
Gurumo
ambaye alizaliwa 1940 alianza muziki mwaka 1959 akiwa na bendi ya
Kilimanjaro Chacha Band. Sasa ni takriban miaka 45, umri wa baba mwenye
wajukuu lakini alichofanikiwa ni kujenga nyumba mbili na kupata shamba
moja. Gari lenyewe alizawadiwa na Diamond mwaka huu baada ya kulalamika
sana kwenye vyombo vya habari.
Nini Tatizo
Maalim
Gurumo (Kamanda), analalamika kuwa wanamuziki wa kizazi kipya
wanasifiwa sana na vyombo vya habari. Akisisitiza kuwa hawana ubunifu,
nyimbo zao hazina athari katika jamii na hudumu chini ya mwaka mmoja
zinapoteza taswira.
Lakini
amesahau kuwa wanamuziki wa sasa wengi wamejiajiri, kipindi hicho bendi
nyingi zilimilikiwa na kampuni, taasisi ama mtu ambaye anapenda sanaa
hiyo ya muziki.
Lakini sasa wanamuziki wameamka, wanajimiliki wenyewe pesa wanazopata zinaingia mifukoni mwao.
Mathalan
tangu Diamond aanze kuimba ameshaingia zaidi ya mikataba kumi tofauti
ambayo ilimnufaisha yeye kama Diamond, matamasha yake yanamnufaisha
yeye, kikundi anachomiliki anakilipa kiasi wanachokubaliana kutokana na
uwezo wa mwanakikundi.
Mwaka
jana, 2012, Diamond aliingia mkataba na kampuni ya I-View Studios wa
kusimamia kazi zake zote kwa miaka miwili. Huu ni mkataba ambao
umemjengea heshima kubwa sana. Ingawa kiasi cha malipo kilifanywa siri
lakini inaonekana ni mkataba mnono.
Kampuni
nyingine ya One Touch, ilifunga naye mkataba wa kuwa wasemaji wake.
Yaani kila anachotaka kufanya ama kuzungumza kwenye jamii, ikiwa kuna
kampuni inataka kufanya naye mazungumzo ya kibiashara, One Touch Company
ndio watakaofanya kazi hiyo.
Hilo
tu linamfanya Diamond awe na uwezo mkubwa wa kupata fedha kutokana na
muziki. Mara nyingine msanii anashindwa kujua thamani yake, anaweza
kutaja kiasi kidogo cha fedha katika ‘dili’ kubwa. Lakini kwa kupata mtu
wa kukusimamia kwenye mazungumzo ya kifedha lazima uwe tajiri.
Aidha,
bendi ambazo Maalim Gurumo amehama kutokana na sababu za kimaslahi
hazipungui kumi, alianza na Kilimanjaro Chacha Band, Kilwa Jazz Band,
NUTA Jazz Band, Mlimani Park, Safari Sound Ochestra, Rufiji Jazz, na
nyingine nyingi kabla ya kumalizia muziki kwenye bendi kongwe ya Msondo
Ngoma Music Band.
Kote
huko alizunguka kwa kutumia kichwa kitupu kujadili thamani ya sauti
yake, hakuwa na mshauri wa masuala ya muziki ambaye atamwambia kutokana
na thamani yako usikubali kuhama bendi hii ili kuenda bendi nyingine
bila kupewa kiasi fulani cha fedha.
Aliweza
kuitwa baa akawa anakunywa bia na nyama choma huku anajadili
mustakabali wa maisha yake na mkurugenzi wa bendi pinzani na anayofanyia
kazi.
Katika
mazungumzo yake na wanahabari Maalim Gurumo aliwahi kutamka kuwa
anatamani siku zirudi nyuma ili anufaike na muziki wake. Lakini nakataa,
hata awe vipi kutokana na mfumo anaoutumia hawezi kuwa tajiri kama
Diamond.
Leo
hii, Maalim Gurumo akiandaa tamasha na kuingiza Sh Mil 50, basi
atakachoambulia ni asilimia 10 ya mapato ambayo ni Sh Mil 5, ambacho
kitakuwa ni kiasi kikubwa kuwahi kukipata kwa tamasha moja tangu aanze
kuimba.
Lakini
siku hiyohiyo Diamond akialikwa katika tamasha hilo la Gurumo ataondoka
na Sh Mil 8 taslimu bila kupungua senti. Bado tofauti ipo kubwa.
Aidha,
mbali ya mapato ya stejini lakini Diamond ana mikataba minono na
makampuni ya simu ambayo yanatumia nyimbo zake kama miito ya simu, ana
mkataba mwingine mnono na kampuni ya Vodacom, ana mkataba na kampuni ya
vinywaji baridi ya Coca Cola hata kufikia kujiita Coke Boy.
Tukiwakusanya
wanamuziki wa zamani kuanzia Mbaraka Mwinshehe mpaka kufikia Maalim
Gurumo, bado hawawezi kufikia mafanikio ya muda mfupi aliyoyapata kijana
mdogo Naseeb Abdul ‘Diamond’ ambaye hata ladha ya ndoa hajaionja
kutokana na umri wake kuwa mdogo.
Wakati
Gurumo akijisifia nyumba mbili alizojenga kwa tamu, Diamond ana nyumba
zaidi ya mbili ambapo moja amemjengea mama yake yenye thamani inayofikia
zaidi ya Sh Mil 50.
Pengine Gurumo ni mwanamuziki bora zaidi kuliko Diamond lakini mwenziye amemzidi kwenye ujanja wa kutafuta fedha
-muhariri wa gazeti la Raia Mwema
Post a Comment